TTCL YAZINDUA HUDUMA YA 4G LTE MBEYA



Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,William  Paul Ntinika akitoa hotuba ya uzinduzi wa huduma mpya ya mawasiliano ya 4G inayotolewa na kampuni ya simu Tanzania ya TTCL kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu Tanzania (TTCL)Waziri Kindamba akielezea umuhimu ya kuzindua mfumo mpya wa mawasiliano wa 4G kwa Mkoa wa Mbeya katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Ofisi za TTCL mkoa wa Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya William Paul Ntinika akisaidiana na Afisa Mtendaji mkuu wa TTCL Waziri Kindamba kutoa kitambaa kuashiria kuzindua  huduma ya 4G mkoani Mbeya.
Afisa mtendaji mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba akimkabidhi zawadi Mkuu wa Wilaya ya Mbeya William Paul Ntinika baada ya kuzindua huduma ya 4G LTE mkoani Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya William Paul Ntinika akisaidiana na Afisa Mtendaji mkuu wa TTCL Waziri Kindamba kuonesha bango  kuashiria kuzindua  huduma ya 4G mkoani Mbeya.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mbeya pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia uzinduzi wa 4G LTE mkoani Mbeya.
Baadhi ya Wageni waalikwa na wateja wa huduma ya simu ya TTCL wakifuatilia uzinduzi wa huduma ya 4G LTE
Baadhi ya Watumishi wa Kampuni ya Simu ya TTCL Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye uzinduzi wa huduma ya 4G LTE mkoani Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya William Paul Ntinika akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kapuni ya Simu ya TTCL Mkoa wa Mbeya,
Afisa wa TTCL akitoa maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na TTCL ikiwemo huduma ya TTCL PESA iliyozinduliwa hivi karibuni.


on

KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imezindua huduma mpya ya mawasiliano ya 4G LTE pamoja na kutambulisha huduma nyingine ya TTCL PESA.

Hata hivyo katika uzinduzi huo imeelezwa kuwa mawasiliano bora yanahitajika ili kuendelea kuimarisha shughuli za kiuchumi mkoani Mbeya  ikiwa ni pamoja na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa taarifa za masoko na bei nzuri kwa wazalishaji na Wakulima.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla wakati akizindua huduma mpya ya kampuni ya Simu ya TTCL ya 4G LTE katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntika katika ofisi za Kampuni hiyo zilizopo jijini Mbeya.

Alisema mawasiliano bora yanamchango mkubwa katika ukuaji wa sekta za Elimu, Afya, Miundombinu, Biashara, utalii, huduma za jamii na sekta zingine mtambuka hivyo kitendo cha TTCL kuibuka upya kutasaidia kuchochea maendeleo katika Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.

Aliongeza kuwa mbali na Mawasiliano kusaidia kukuza uchumi pia Wafanyakazi wa Sekta binafsi na sekta za umma wanahitaji mawasiliano bora ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo yao ya kazi.

Aidha alitoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuchangamkia fursa za kibiashara zinazotolewa na TTCL kama vile kuwa wakala wa kuuza vocha, Laini na kuwa Wakala wa huduma mpya ya kifedha ya TTCL Pesa kwani kufanya hivyo kutasaidia kuongeza ajira na vipato vyao.

Hata hivyo Makalla alitoa wito kwa Kampuni ya TTCL kupanua wigo wa utoaji huduma kwa kuhakikisha huduma hiyo inasambaa kote nchini hususani vijijini ambako watumiaji ni wengi ambao pia wanahitaji huduma zenye gharama nafuu kama zinazotolewa na kampuni ya TTCL.

Awali Afisa mtendaji mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba katika hotuba yake alisema Kampuni ya TTCL ni kampuni ya kizalendo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 hivyo inatekeleza mpango mkakati wa biashara wa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2018 unaolenga kuboresha na kutoa huduma mpya katika soko la mawasiliano nchini.

Kindamba alisema malengo mengine ya mkakati huo ni pamoja na kuongeza tija na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wateja wa mawasiliano ambapo hivi sasa wameweza kufanya mabadiliko mengi yaliyowezesha Kampuni hiyo kurejea kwa kishindo katika soko la mawasiliano.

Alisema mbali na kuzindua huduma mpya ya mawasiliano ya 4GLTE pia ni kutambulisha huduma mpya ya kifedha kwa njia ya mtandao ijulikanayo kama TTCL Pesa ambayo ilizinduliwa Julai mwaka huu na Makam wa Rais Mama Samia Hassan Suluhu.

Alisema huduma hiyo ya kifedha itawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali kama kutuma fedha, kulipia Ankara za maji, umeme, ving’amuzi na kununua vifurushi vya TTCL huku huduma zingine zikiendelea kuongezwa ikiwemo kulipia kodi TRA.

Aliongeza kuwa lengo la kuzindua huduma hizo mkoani Mbeya linatokana na kuwa ni Mkoa wenye kibiashara na utajiri mkubwa wa idadi ya watu na uwepo wa shughuli za kiuchumi zinazogusa sekta nyingi na kuwa kitovu cha kilimo cha kibiashara, tegemeo la chakula nchini na kuwa kituo kikubwa cha kibiashara kutokana na kupakana na Nchi jirani za Malawi na Zambia hivyo TTCL kutumia fursa hiyo ya kiuchumi.

No comments