PROF, MBARAWA AZINDUA BODI MPYA YA TTCL, AITAKA KUJIPANGA KUINGIA KATIKA USHINDANI WA KIBIASHARA
Picha na Frank Shija – MAELEZO
……………………..
Thobias Robert-Maelezo
21, sept 2017
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Mkame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Kampuni ya
Mawasiliano nchini (TTCL) kuhakikisha kuwa inasimamia vyema kazi na majukumu
yake ili kuiwezesha kampuni hiyo kujiendesha kibiashara na kuimarisha huduma za
mawasiliano hapa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi
hiyo Jijini Dar es Salaam jana, Profesa Mbarawa aliitaka TTCL kuchape kazi kwa bidi ili
kurahisisha huduma mbalimbali za kimawasiliano nchini na kuhakikisha kuwa
wanaendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano yenye sera ya hapa kazi tu.
“Nataka bodi mjue tunakwenda wapi
katika kampuni hii lakini pia tunahitaji kufanya kazi kwa juhudi, kushindana na
makampuni mengine ya simu, mhakikishe mapato makubwa yanatoka kwenye data
hali kadhalika tujue mnapaswa mjue strenght (nguvu) yenu iko wapi maana
tusipojibu maswali haya hatuwezi kufanya ushindani na makampuni mengine,”
alifafanua Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa alisema kuwa,
Serikali imeweka sera nzuri za
uwekezaji katika sekta ya mawasiliano kiasi
ambacho kimeongeza mapato pamoja na ushindani wa huduma ya mawasiliano na
kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo hapa nchini.
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa serikali
imefanya mabadiliko yaliyofanywa na serikali ili kuipa nguvu Kampuni ya TTCL
ikiwa ni pamoja na kuondoa ubia wa umiliki wa TTCL na wawekezaji asilimia 35 na
kuzirejesha serikalini, kujenga mkongo wa taifa wa mawasilino, kujenga kituo
cha taifa cha kuhifadhi kumbukumbu (Data center) pamoja na kulipa madeni ya
kampuni hiyo.
Aidha Prof. Mbarawa ameitaka Bodi ya
Wakurugenzi kuhakiksha kuwa TTCL inaleta mabadliko na maendeleo katika kufikia
sera ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda, kuongeza wateja na
watumiaji wa huduma zitokanazo na TTCL, kuwafikia watumiaji wengi zaidi nchini
kote na kuendelea kuwa kampuni bora ya mawasiliano.
Prof. Mbarawa aliongeza kuwa, TTCL ni
lazima wabadilike katika utoaji wa huduma zake, ili kuendana na manadiliko ya
teknolojia ambapo amewaeleza kuwa kwenye sekta ya mawasiliano mambo yanabadilika
kila siku, sekta inakua haraka na hata uendeshaji wake unabadilika.
“Mathalani ukiangalia makampuni makubwa
kwa sasa, mapato yao yamebadilika kutoka kwenye sauti hadi data pamoja na
miamala ya pesa hivyo TTCL wanapaswa wajipime waangalie uwezo wao uko wapi na
nguvu zao ziko wapi ili waweze kujipanga vizuri kuhakikisha wanashindana na
makampuni mengine ya mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Prof. Mbarawa.
Awali akizungumza katika hafla hiyo,
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mhandisi Omary Nundu, alisema kuwa tangu
ateuliwe katika bodi hiyo mambo mengi wameyafanya hadi sasa ikiwemo
kuifufua kampuni hiyo, kushirikiana na wadau wengine wa mawasiliano pamoja
na kuanzisha TTCL Pesa.
“Kwa sasa tunahudumia watu laki tatu
hapa nchini, lakini tumenuia mwisho wa mwaka huu wa fedha 2017/2018 tufikie
wateja milioni moja na baada ya miaka mitano yaani ifikapo 2021/2022 tuwe na
wateja milioni tano ambapo tutakuwa tumefikia asilimia 10 ya wateja wa soko la
mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Mhandisi Nundu.
Aidha, Mhandisi Nundu aliendelea kusema
kuwa mwaka 2016, TTCL ilipata bilioni 0.21 katika soko lake na zaidi mwaka huu
wanatarajia kupata bilioni 0.3 na kwamba wanatarajia kupata faida ya zaidi ya
bilioni 40 ifikapo 2022 baada ya makato ya kodi.
“Katika kuyafanikisha matarajio yote
haya, tunapaswa kupata jumla ya dola za kimarekani milioni 673,
ambapo dola milioni 300 tunatarajia kuzipata kama mtaji wa uwekezaji kutoka
serikalini, huku kampuni ikitafuta njia nyingine za kuapata fedha zilizobaki katika
mpango na matarajio yetu,” alifafanua Mhandisi Nundu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Mawasiliano Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Mary Sassabo alisema
sekta ya mawasiliano ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi kwa kurahisisha
mawasiliano ya kati ya mtu na mtu na taifa kwa ujumla kwa kurahisisha
usambazaji na upatikanaji wa huduma na bidhaa kutoka sehemu moja na nyingine.
“Sera ya serikali ya kuelekea uchumi wa
viwanda inatoa fursa kubwa kwa sekta ya mawasiliano kukua, pia ukuaji wa
shughuli za uchumi unachochea mahitaji ya mawasiliano kuongezeka ikiwemo
serikali mtandao, tiba mtandao, elimu mtandao, biashara mtandao, utangazaji
mtandao kwa njia ya runinga na radi,” alifafanua Dkt.Sassabo.
Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL iliteuliwa
rasmi mwezi Februari 2017,na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli ikiwa ni jitihada za kufufua na kurejesha kampuni hiyo katika
ushindani, kusimamia mawasiliano yote ya serikali na kujiendesha kwa faida. Kwa
sasa serikali inajiandaa kupeleka muswada bungeni ili kuirasimisha
TCCL iwe na bajeti ya kujitegemea.
kwa mahitaji ya greencard, passport size,passport za kusafiria visafoto.com ni bora katika uandaaji
ReplyDelete