SERIKALI NA TTCL KUMILIKI KWA PAMOJA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiweka saini kitabu cha Wageni alipotembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoa wa Kigoma. 
 Baadhi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoani Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) alipotembelea ofisi hizo. 
Baadhi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Mkoani Kigoma wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) alipotembelea ofisi hizo. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na 


Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa TTCL Kigoma alipotembelea ofisi hizo. Wengine waliokaa kutoka kushoto ni Meneja wa TTCL Kigoma, Bw Lugage Abdallah, Kaimu Mkuu wa Mkoa Kigoma, Bw Saveli Maketa, Mbunge wa Kigoma Mjini Zito Kabwe na Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura. 

SERIKALI kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), zitamiliki kwa pamoja Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ili kuongeza ufanisi wa mkongo huo katika kutoa huduma za mawasiliano nchini.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amesema, Serikali ipo tayari kushirikiana na kampuni ya TTCL katika kuumiliki Mkongo huo kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na TTCL tangu mwaka 2010 ilipopewa jukumu la kuujenga, kuusimamia na kuuendesha Mkongo huo.


Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo alipotembelea Ofisi za Kampuni ya Simu TTCL Mkoa wa Kigoma ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 5 Mkoani humo kukagua shughuli za Taasisi zilizo chini ya Wizara yake.


Mhe Mbarawa alisema, Ombi lililotolewa na TTCL la kumiliki mkongo lina mantiki kubwa kutokana na uwezo wa kiufundi, kitaalamu na kiundeshaji uliopo ndani ya kampuni hiyo lakini kutokana na Sababu za kiserikali, ni lazima Serikali ibaki kuwa na mkono wake ndani ya Mkongo ili kuudhibiti, kuulinda kuhakikisha kuwa unatumika kwa tija na kufanya kazi zake kwa ufanisi.


"Tutaendelea kuzungumza Serikalini ili tukubaliane mgawanyo wa asilimia katika Mkongo wa NICTBB. Sina tatizo kuipa Ttcl asilimia hadi 70 na Serikali ibaki na asilimia 30. Cha msingi hapa ni kwamba lazima Mkono wa Serikali uwepo.. Huu ndio msimamo wangu kwa sasa, tutaendelea kujadiliana ili tuwe na namna bora zaidi ya kutekeleza mpango huu. Nia yangu na wenzangu wote Wizarani na Serikalini kwa ujumla, ni kuhakikisha Ttcl inaimarika na kuwa kinara katika huduma za Mawasiliano nchini" amesisitiza Mhe Mbarawa.


Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT, Wazalendo), Mhe Zito Kabwe alieongozana na Waziri Mbarawa katika ziara hiyo alisema, TTCL imeonesha uwezo mkubwa na jitihada za dhati tangu ujenzi hadi kuuendesha Mkongo kwa niaba ya Serikali na kushauri kuwa, wakati umefika kwa TTCL kukadhiwa mamlaka ya miundombinu hiyo ili kuipa TTCL nguvu zaidi na uhuru katika kuendesha chombo hicho.


"...Kwa maoni yangu, TTCL inastahili kukabidhiwa Mkongo wa NICTBB, wakipata mkongo huu wataimarika sana. Nimekuwa nikishauri mara zote kuwa, tukikabidhi Mkongo kwa TTCL tunaweza hata kuwapa jukumu moja tu la kufanya biashara ya Data, wakaachana na biashari nyingine ili waendeshe Mkongo kwa ufanisi" amesema Mhe Zito.


Kwa Upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema, kampuni ya TTCL inaishukuru Serikali kwa nia njema ya kutaka kuimilikisha kampuni hiyo sehemu ya Mkongo kwa kuwa ni jambo lenye tija kibiashara na kuthamini juhudi kubwa na moyo wa uzalendo ulioneshwa na Wafanyakazi wa TTCL katika kuujenga na kuuhudumia Mkongo tangu kuanzishwa kwake.


Awali, Katika taarifa yake kwa Mhe Waziri, Meneja wa TTCL Mkoa wa Kigoma, Bw Lugage Abdallah alisema, Kampuni hiyo imejipanga kuongeza ufanisi kwa kuboresha huduma, kuongeza idadi ya Wateja na kutatua kwa haraka matatizo ya kiufundi yanapojitokeza ili kuwapa wateja huduma za uhakika.


"Mhe Waziri, tunakabiliwa na changamoto kubwa ya Uharibifu wa Miundo mbinu ya TTCL na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Tunashirikiana na jamii na vyombo vya Ulinzi na Usalama kulinda miundo mbinu yetu na juhudi zimeanza kuzaa matunda kwa kukamata Wahalifu. Ombi letu kubwa kwako ni kuisaidia TTCL hasa katika kupata malipo ya huduma tunazotoa kwa Taasisi za Umma ambazo zimekuwa ni wadaiwa sugu" alisema Bw Abdallah.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amekamilisha ziara yake Mkoani Kigoma Jumamosi Aprili 02 na kuelekea Mkoani Katavi kwa ziara kama hiyo

Michuzi 

No comments